Skip to main content Skip to footer

Kupotea kwa Serengeti - Ardhi ya Wamaasai

May 15, 2018
Source
Deutsche Welle

Ripoti mpya iliyotolewa na Taasisi ya Oakland mjini Carlifonia nchini Marekani inafichua jinsi kampuni zinazoratibu safari za watalii zinavyotumia machafuko na vitisho kudhibiti ardhi nchini Tanzania.

Ripoti hiyo iliyopewa jina "Losing the Serengeti, The Maasai Land that was to be run forever - Kuipoteza Serengeti - Ardhi iliyotakiwa kuwepo milele, inaziangazia kampuni mbili moja ikiwa ni Ortelo Business Corporation, OBC, kampuni inayoendesha shughuli za uwindaji wa wanyamapori kwa niaba ya familia ya kifalme yenye makao yake makuu katika Umoja wa Falme za Kiarabu, na nyingine ni Tanzania Conservation Limited, TCL, ambayo ni kampuni ya biashara inayoratibu safari za watalii inayoendeshwa na wamiliki wa kampuni ya Thomson Safari yenye makao yake mjini Boston nchini Marekani.

Suala nyeti linaloibua wasiwasi ni kwamba jamii ya Wamasai wana haki waliyorithi ya umiliki wa ardhi ya Serengeti, neno la kimasai ambalo maana yake ni ardhi iliyotakiwa kuwepo milele. Swali linaloulizwa katika ripoti hiyo ni vipi haki hiii ilivyokanyagwa na kunyimwa Wamasai, kiasi kwamba leo hawaruhusiwi hata kulima na kupanda vyakula katika mashamba madogo karibu na nyumba zao, jambo linalosababisha njaa inayoenea, utapiamlo na magonjwa. Hawana tena maeneo ya malisho kwa ajili ya mifugo yao. Ghafla mambo yamebadilishwa na swali linaloulizwa katika ripoti hiyo ni nani aliyepitisha maamuzi hayo, kufikia kiwango cha Wamaasai wakati mwingine kupewa vibaruwa na ajira katika kambi za watalii.

Anuradha Mittal, Mtafiti Mwandamizi wa taasisi wa Oakland mjini Carlifonia aliyehusika kufanya utafiti nchini Tanzania alisema, "Ripoti hii inaangazia jinsi Wamaasai wa Tanzania wanavyokabiliwa na ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo vitisho, kufukuzwa kwa nguvu kutoka makao yao, kukamatwa, kupigwa, na njaa. Na hii ni kutokana na sera za serikali ya Tanzania na baadhi ya makampuni yanayoratibu safari za watalii yanayoendesha shughuli zake nchini humo."